Simba yaining’iniza Yanga usiku


kocha Patrick Phir

YANGA imemfikiria Emmanuel Okwi na Dan Sserunkuma wa Simba kisha ikatikisa kichwa, ikapiga hesabu zake za haraka jinsi ya kuokoa jahazi kwenye Mtani Jembe Jumamosi ni kusajili fowadi asiye na masihara na anayekubalika na Marcio Maximo ambaye ni Danny Mrwanda.
Simba nayo ikakaa ikaona Joseph Owino anazingua kurudi kambini kwa wakati ikaagiza kifaa kingine matata zaidi kutoka Kenya ambacho ni David Owino wa Gor Mahia aliyewasili kambini jana mchana na jioni akaanza kupasha tizi na timu mjini Unguja, Zanzibar huku viongozi wakisisitiza kwamba Yanga lazima ining’inie Uwanja wa Taifa.
Joseph Owino alichelewa kuripoti kwenye kambi ya timu hiyo hivyo kuwaweka katika wakati mgumu kocha Patrick Phiri na viongozi, hata hivyo naye aliwasili jana. Viongozi hao wanadai kwamba Owino si mzuri pale anapochelewa kujiunga na timu kutokana na kucheza soka la kufundishwa zaidi kuliko la kujiongoza hivyo anaweza kuigharimu Simba kwenye mechi hiyo na wanampa nafasi hiyo David Owino ili kujiweka katika nafasi salama ya kutofungwa na Yanga.
Wiki hii vigogo wa Simba walikuwa wanahaha kufikia makubaliano ya mwisho na beki huyo matata ambaye anataka apewe dola 52,000 (Sh 88.5 milioni) ili asaini mkataba wa kuichezea Simba japokuwa ana dili lingine la kwenda kucheza Finland.
“Ijumaa (kesho) ndiyo itajulikana nani ataachwa na nani atabaki, lakini endapo David tutakubaliana naye basi kati ya Joseph au Pierre Kwizera mmoja wapo lazima aondoke ingawa hata Amissi Tambwe yupo katika hatari hiyo,” alisema kiongozi mmoja wa usajili wa Simba.
Raphael Kiongera na Donald Mosoti ambao wote ni Wakenya walisema kuwa David ni beki bora na endapo atasajiliwa atakuwa na uhakika wa kucheza kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo.
“Wakimpata David watakuwa wamelamba dume, ni mchezaji mzuri ambaye anaweza kucheza beki yoyote pale nyuma, Simba wanatakiwa kuhakikisha wanampata beki huyo atatusaidia, ni mzuri. Ninasema hivyo kwa sababu nimemuona na nimecheza naye, anazuia, anakaba na ana kasi,” alisema Kiongera ambaye ni mshambuliaji ingawa kwa sasa hana nafasi katika kikosi cha Phiri kwani ni majeruhi na tayari amefanyiwa upasuaji wa goti.
Kwa upande wa Mosoti ambaye alionekana kushangazwa na habari hizo, alisema: “Aise David Owino anaenda Simba! Aise ni bonge la beki, wamchukue atawasaidia kwani anaweza sana.”
David aliliambia Mwanaspoti kuwa “Bado tupo kwenye mazungumzo,tukifikia makubaliano nitacheza Simba.”
Kocha wa Simba, Patrick Phiri alilsema: “Najua uwezo wake ndio maana naamini moja kwa moja kuwa tatizo hilo la ulinzi litakwisha Simba.”

No comments