Ndicho kilichojiri... Mtani jembe


 Simba ndiye Mtani Jembe



KLABU ya soka ya Simba imeendelea kuushikilia ubingwa wa mchezo wa
Nani Mtani Jembe baada ya kuwafunga watani zao Yanga mabao 2-0
KLABU ya soka ya Simba imeendelea kuushikilia ubingwa wa mchezo wa Nani Mtani Jembe baada ya kuwafunga watani zao Yanga mabao 2-0, katika mchezo mkali na kusisimua uliofanyika kwenye uwanja wa taifa Dar es Salaam.
Ushindi huo ni wapili mfululizo kwa Simba ambayo iliuanza mchezo huo taratibu sana kabla ya kuzinduka kuanzia dakika ya 30 na kufanikiwa kupata ushindi huo ambao umeisaidia timu hiyo kurudisha imani kwa mashabiki wake ambao walikuwa wamepoteza matumaini.
Yanga iliyokuwa ikipewa nafasi kubwa ya kuibuka na ushindi katika mchezo wa ndiyo iliyokua ya kwanza kulifikia lango la Simba na kufanya shambulizi kali dakika ya kwanza lakini wakashindwa kuitumia vizuri nafasi aliyopata Mbrazili Andrew Coutinho.
Simba ilijibu mapigo katika dakika ya tatu ambapo nahodha wake Emmanuel Okwi, aliachia shuti kali lakini halikuweza kulenga lango na kutoka nje na kuwa golikiki.
Baada ya shambulizi hilo Simba ilionekana kupotea kabisa na kuwaacha wapinzani wao Yanga kuutawala mchezo huo na kutengenza mashambulizi mengi kupitia kwa mshambuliaji wake mpya raia wa Liberia Kpah Sean Sherman, aliyekuwa akiwasumbua sana mabeki wa Simba katika mchezo huo.
Mshambuliaji huyo aliyesaini mkataba wa miaka miwili kuwachezea vijana hao wa kocha Marcio Maximo, alizidi kuonyesha uwezo wake katika dakika ya nane ya mchezo baada ya kuwalamba chenga mabeki wa Simba na kupiga shuti kali lililopanguliwa na kipa Ivo Mapunda na kuwa kona isiyokuwa na faida.
Katika dakika ya 11 mpambano huo ulilazimika kusimama kwa muda baada ya kutokea vurugu zilizotokana na Okwi, kumchezea vibaya Juma Abduli wa Yanga na Kelvini Yondani kumsukuma chini mshambuliaji huyo na kuzua tafrani kubwa uwanjani hapo.
Mchezo huo uliendelea kuwa wa ushindani mkubwa huku wachezaji wa timu hizo wakioneshana ubabe kwa kuchezeana rafu ambazo zilisababisha Elias Maguli kuonyeshwa kadi ya njano dakika ya 21.
Mambo yalionekana kubadilika kuanzia dakika ya 30 baada ya Simba kupata bao la kwanza lililofungwa na Awadhi Juma aliyemalizia mpira wa adhabu ndogo uliokuwa umepigwa na Okwi kutemwa na kipa wa Yanga Deogratius Munish ‘Dida’ na kuukwamisha wavuni.
Kuingia kwa bao hilo kulionekana kuichanganya Yanga na kuzidi kupoteana huku wapinzani wao Simba wakionekana kuimarika na kuutawala mchezo huo na kutengeneza nafasi nyingi ambazo washambuliaji wake Simon Sserunkuma na Elias Maguli walishindwa kuzitumia ipasavyo.
Wakati ikionekana kana kwamba Simba itakwenda mapumziko ikiwa na bao hilo moja Maguli aliwainua vitini mashabiki wa timu yake baada ya kufunga bao la pili akimalizia mpira uliogonga mwamba wa pembeni uliokuwa umepigwa na Sserunkuma.
Mpira huo ulitokana na mpira uliorushwa na beki wa kulia Nassor Masoud ‘Chollo’ baada ya beki Oscar Joshua kuutoa mpira huo katika harakati za kuokoa hatari langoni mwao.
Yanga ingeweza kuongezwa bao jingine la tatu kabla ya mapunziko kutokana na wachezaji wake kucheza bila mpangilio lakini walinzi wake Kelvin Yondani na Nadir Haroub ‘Cannavaro waliondosha hatari hizo.
Kipindi cha pili Yanga waingiza Dany Mrwanda na Mrisho Ngasa kuchukua nafasi za Coutinho na Emerson Oliveira, na timu hiyo kuonekana kuimarika na kurudi kasi yake ya awali lakini bado tatizo lilikuwa kuutumbukiza mpira kwenye nyavu za Simba zilizokuwa zinalindwa na Mapunda.
Baada ya kuona mambo magumu Yanga iliwaingiza Mrisho Ngasa na Husseni Javu huku Simba ikiwatoa Ramadhani Singano Juku Musheed na kuwaingiza Said Ndemla na Danny Sernkuma ambao kwa kiasi fulani waliongeza presha ya kuwafanya Yanga kupunguza kasi ya mashambulizi.
Hadi dakika 90 zinakamilika Simba iliweza kuibuka na ushindi huo wa mabao 2-0 na kufanya mashabiki wa timu hiyo kulipuka kwa furaha baada ya kuwafunga watani zao hao.Simba

No comments