Yanga yashusha Wazambia, waja kwa majaribio


Jonas Sakuwaha
KESHO Jumatano Yanga itawashusha nchini wachezaji wanne raia wa Zambia ambao mmoja wao ni kiraka wa TP Mazembe, Jonas Sakuwaha.
Habari za uhakika ambazo Mwanaspoti imezipata jana Jumatatu ni kwamba wachezaji hao watatu wanacheza ligi ya ndani huko kwao, lakini mwenye nafasi kubwa na ambaye Yanga ina malengo naye ni Jonas.
Habari zinasema kwamba mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 31, anaondoka Mazembe kwenda kutafuta changamoto mpya sehemu nyingine kwa vile amekuwa hana nafasi ya kudumu kwenye kikosi cha kwanza wanachocheza Watanzania, Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu.
Mmoja wa vigogo wa usajili wa Yanga aliidokeza Mwanaspoti kwamba endapo mchezaji huyo atafuzu majaribio na kukubalika na Marcio Maximo huenda Hamis Kiiza akaonyeshwa mlango wa kutokea kurudi kwao Uganda.
Kiiza amekuwa hana wakati mzuri mbele ya Maximo ingawa dakika chache anazochezeshwa huonyesha makali ya aina yake. Baada ya kumtema Genilson Santos ‘Jaja’, wachezaji wa kigeni waliosalia Yanga ni Mbuyu Twite, Andrey Coutinho, Kiiza na Haruna Niyonzima. Timu hiyo pia imetangaza ujio wa Mbrazili Emerson De Oliveira Neves Rouqe kwa majaribio ambapo atatua nchini kesho saa saba mchana sambamba na Maximo.
Mbali na wachezaji hao wawili wa kigeni wanaokuja kwa majaribio, Yanga tayari imeshafanya mazungumzo ya awali na straika wa Uganda na AS Vital, Yunus Sentamu. Kikanuni Yanga ambayo imeanza mazoezi jana jijini Dar es Salaam inapaswa kuwa na wachezaji watano wa kigeni hivyo benchi la ufundi litalazimika kufanya uamuzi mgumu.

No comments