Serikali yataja tarehe ya kujiandikisha


Aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha ili kuwachagua viongozi wanaowataka kwenye vijiji, vitongoji na mitaa.
Wananchi wametakiwa kujitokeza kujiandikisha katika daftari maalumu la kupigia kura kuanzia Novemba 23 hadi 29 kwa ajili ya kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Mkurugenzi wa Serikali za Mitaa katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Tamisemi, Kharist Michael Luanda alisema wananchi wanaotaka kuwania nafasi mbalimbali za uongozi katika ngazi za vijiji, vitongoji na mitaa wanapaswa kuchukua fomu za kugombea kuanzia Novemba 16 hadi 22.
Aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha ili kuwachagua viongozi wanaowataka kwenye vijiji, vitongoji na mitaa.
Alisema uandikishaji huo utafanyika katika vituo maalumu vilivyoandaliwa ambavyo vipo katika majengo ya umma kuanzia saa 1.30 asubuhi na kufungwa saa 10.30. Alisema katika sehemu ambazo hazina majengo, uandikishaji utafanyika katika vituo maalumu kutokana na makubaliano ya msaidizi wa uchaguzi na viongozi wa vyama vya siasa.
Alisema vyama vya siasa vitaruhusiwa kuweka mawakala wakati wa uandikishaji wa wapigakura lakini gharama za kuwalipa zitakuwa juu ya chama husika. Kuhusu sifa za anayetaka kuwania nafasi katika ngazi hizo, mkurugenzi huyo alisema ni lazima awe Mtanzania mwenye miaka 21 au zaidi na awe mkazi wa kudumu wa eneo husika.
Alisema wasimamizi wasaidizi wa kila kituo wanapaswa kubandika orodha ya wapigakura ifikapo Novemba 30 na endapo mkazi yeyote au chama cha siasa kitakuwa na pingamizi au maoni juu ya orodha hiyo, awasiliane na msimamizi msaidizi wa uchaguzi ili kufanya marekebisho na orodha ya mwisho itabandikwa siku tatu kabla ya uchaguzi.
Viongozi watakaochaguliwa katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa ni wajumbe wa halmashauri ya kijiji wasiopungua 15 na wasiozidi 25, wenyeviti wa mitaa na wajumbe wa kamati za mitaa wasioziidi sita na wenyeviti wa vitongoji.
Gharama za uchaguzi
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliopangwa kufanyika Desemba 14, utagharimu Sh20 bilioni.
Kiasi hicho kinajumuisha maandalizi ya uchaguzi huo, elimu kwa wapigakura, matangazo, wasimamizi, vifaa na gharama za uandikishaji na usafirishaji wa vifaa.
Luanda alisema hadi jana utaratibu ulikuwa ukiendelea vizuri.

CUF, Chadema walia

No comments