Mambo yaiva Msimbazi


Dann Sserunkuma
SIMBA imeendelea na mazoezi yake ya gym na mazoezi mepesi ya uwanjani ambayo yanafanyika Uwanja wa TCC Chang’ombe na Jumatatu ijayo wataingia kambini jijini Mwanza tayari kujiweka sawa na mechi ya Nani Mtani Jembe dhidi ya Yanga Desemba 13.
Lakini kama hilo halitoshi,  habari za ndani ya kamati ya usajili zinasema wamemshusha nchini straika Dann Sserunkuma wa Gor Mahia ya Kenya kwa siri kubwa ambapo leo huenda akapimwa afya na kutambulishwa rasmi kwa waandishi wa habari.
Habari za ndani zinadai kwamba Simba wenyewe wamekuwa wakifichana siri hiyo kwa kuhofia hujuma ambazo zinaweza kufanywa na Yanga.
 Katika mazoezi ya jana Alhamisi iliwakosa wachezaji wake nyota Emmanuel Okwi na Joseph Owino ambao wanatarajiwa kuwasili nchini leo Ijumaa licha ya kwamba tangu Jumatatu walitakiwa wawepo.
Okwi na Owino ni raia wa Uganda ambapo walikwenda kwao kwa ajili ya mapumziko mafupi. Kocha wao Mzambia Patrick Phiri naye anatarajia kuwasili leo huku kambi ya timu hiyo imepangwa kuanza Jumatatu ikiwa ni maandalizi ya mechi yao dhidi ya Yanga ya Nani Mtani Jembe.
Wachezaji wengine ambao hawakuwepo kwenye mazoezi hayo ni mlinda mlango Ivo Mapunda ambaye amefiwa na mama yake mzazi. Ivo aliondoka jana Alhamisi kuelekea msibani Mbeya.
Wengine ni Awadh Juma, Nasoro Masoud ‘Chollo’ na Abdul Makame waliopo timu ya taifa ya Zanzibar, Elius Maguli na Uhuru Seleman ambao walikuwa na udhuru. Kipa Hussein Shariff ‘Casillas’ yeye ni majeruhi ingawa ameanza mazoezi mepesi, Haruna Chanongo alisimamishwa na viongozi wake ambapo suala lake bado halijajadiliwa.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ivo alisema kuwa mama yake alifariki ghafla usiku wa kuamkia jana Alhamisi ambapo atajua zaidi taratibu za mazishi akifika kwao Tukuyu, Mbeya.
“Nipo nashughulikia safari ya kwenda msibani nimefiwa na mama yangu, hajaumwa ni kifo cha ghafla hivyo nitajua zaidi nikifika huko,” alisema Ivo ambaye pia hivi karibuni alifiwa na baba yake mzazi.
Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Seleman Matola alitamba kuwa mechi hiyo ya Nani Mtani Jembe watashinda kama ilivyokuwa mechi ya mwanzo ambapo walishinda bao 3-1 ambapo mawili yalifungwa na Amissi Tambwe na jingine lilikuwa la Awadh Juma. Bao la Yanga lilifungwa na Okwi ambaye sasa anaichezea Simba.
“Sisi ni mabingwa wa mechi hiyo, hivyo tunawaomba mashabiki kuungana kwa pamoja ili kutetea ubingwa huo na kuweka kando tofauti zilizopo, Okwi na Owino tuliwapa taarifa ya kuanza kwa mazoezi lakini bado hawajafika na tumepeleka taarifa kwa viongozi wetu ambao watashughulikia hilo,” alisema Matola.
Msemaji wa Klabu hiyo Humphrey Nyasio akifafanua juu ya wawili hao alisema: “Okwi na Owino tunatarajia kuwa watawasili kesho (leo Ijumaa) pamoja na kocha,  kuna taratibu zilikuwa zinafanywa juu ya safari zao, wengine wapo timu ya taifa ya Zanzibar na Ivo amefiwa na mama yake.

No comments