MAMBO YA KUZINGATIA KABLA YA KUMRUDIA MPENZI WA ZAMANI!

Nisiku nyingine tena tunakutana katika safu hii
nikiamini umzima na unaendelea vizuri na
majukumu yako ya kila siku kama kawaida
.Mimi namshukuru Mungu kwa kila jambo,
amenijaalia afya njema na nguvu za kutosha
kiasi cha kuweza kukuandikia wewe kile
ambacho naamini kina umuhimu katika maisha
yako ya kimapenzi.
Leo ningependa tuzungumzie mambo ya
kuzingatia kabla ya kumrudia mpenzi ambaye
aidha mmeachana, yupo mbali na wewe au
umepoteana naye kwa muda mrefu.
Kugombana ni sehemu ya maisha ya
mwanadamu. Yawezekana ulikuwa na mwenzi
wako ambaye ulimpenda kwa moyo wako wote
na sasa mmeachana lakini moyo wako bado
unahitaji kuwa naye.
Kutengana kuna mambo mengi, wakati mwingine
huenda ilikuwa ni hasira tu. Siku zote baada ya
hasira kuisha, moyo hubaki peke yake katika
nafasi yake halisi ya kufanya maamuzi.
Hapo ndipo penye lengo la mada yetu ya leo.
Kwamba, kwa msingi huo umegundua kumbe
mpenzi wako uliyeachana naye, bado
unampenda.
Kwamba hata makosa aliyokuwa akiyafanya,
ulimsababishia au si makubwa kiasi cha
kuachana na badala yake mnaweza kukaaa na
kuzungumza kiutu uzima na kuyamaliza.
Upo tayari rafiki? Je, uko katika kundi hilo?
Unataka kumrudisha mpenzi wako wa zamani?
Kama jibu ni ndiyo basi mada hii inakuhusu.
HAKIKISHA BADO ANAKUPENDA
Kwa utafiti mdogo nilioufanya nimebaini kuwa
baadhi ya watu huamini kwamba kurudi kwa
mara nyingine kwa mpenzi wa zamani ni
kujidhalilisha, kujishusha na kujisalimisha.
Hilo si kweli hata kidogo, kikubwa cha kuzingatia
hapa ni moyo. Je, unahisi bado unampenda? Ni
kweli naye anakupenda? Kama sifa hizi zipo,
hayo mambo madogo ambayo mmetofautiana ni
ya kawaida kabisa ambayo mnaweza
kurekebishana taratibu.
Kwa msingi huo basi, hakuna tatizo lolote katika
kurudiana na mpenzi wako wa zamani, maana
tayari mmeshajuana vya kutosha, hivyo kukupa
urahisi wa kufanya yale anayoyapenda na
kuepuka asiyopenda, jambo litakalozidisha umri
wa uhusiano wenu.
HAJAPATA MWINGINE?
Lazima ujue kuhusu historia yake kiuhusiano
baada ya kuachana na wewe. Hapo unatakiwa
kufanya ushushushu wako kimyakimya bila yeye
kujua. Ikiwa ameshatembea na mwingine, maana
yake ni mtu asiye na msimamo na huenda
anaongozwa zaidi na tamaa za kimwili na si
mapenzi ya dhati.
Katika kipengele hiki, ni muhimu sana kujua
kama muda huo ambao wewe unahitaji kurudi
tena mikononi mwake kama ana uhusiano
mwingine. Kimsingi kama atakuwa ndani ya
uhusiano, itakubidi uwe mpole.
Unatakiwa kufanya hivyo kwa sababu anaweza
kukubali kuwa na wewe wakati akiwa bado
hajaachana na mpenzi aliyenaye kwa muda huo,
hivyo wewe kuwa kama mwizi tu kwa
mwenzako.
Hapo utakuwa katika mapenzi ya kushea, jambo
ambalo si zuri kisaikolojia na hata kiafya.
Kumbuka kwamba, unaweza kuwa na mwenzi
wako, mkapendana kwa dhati na mkadumu kwa
muda mrefu, lakini kwa bahati mbaya
mkaachana kwa sababu ambazo mnazifahamu
wenyewe.
Katika muda mfupi ambao utakuwa umeachana
naye, anaweza kufanya mambo ya ajabu sana.
Pamoja na kwamba moyo wako unamhitaji, lakini
anaweza kuwa tayari ameshapoteza sifa za
kuwa na wewe. Katika hali hiyo, ni sahihi
kurudiana naye? Bila shaka jibu hapa ni siyo
sahihi.
ANA DHAMIRA YA NDOA?
Huenda uliachana na mpenzi wako lakini bado
unaamini ndiye alipangwa kuwa mwenza wako
wa maisha, hiyo isiwe sababu, jiulize pia kama
na yeye anahitaji kuingia kwenye maisha ya
ndoa na wewe.
Nasema hivyo kwa sababu, unaweza
kunga’ang’ania kumrudisha mpenzi wako wa
zamani kumbe mwenzako anataka kupitisha siku
tu na wewe. Hana mpango wa kuishi na wewe
kindoa.
Kama utabaini mliachana lakini wote dhamira
yenu ni kuoana, basi mrudie lakini kama unahisi
ni mtu wa kustarehe tu na wewe na wala si
muolewaji/muoaji, sidhani kama itakuwa sawa
kumrudia.
HANA KINYONGO?
Wapo ambao wanafikia hatua ya kuachana
baada kukoseana tena wakati mwingine makosa
makubwa. Kwa maana hiyo kama wewe ndiye
uliyemkosea mpenzi wako kabla ya kuanza
jitihada za kumrudia, kwanza chunguza kama
hana kinyongo na wewe na amekusamehe kutoka
moyoni mwake?
Kama bado ana kinyongo na ukalazimisha
kurudiana naye, huwezi kulifurahia penzi lenu,
itakuwa kila akikumbuka ulivyomkosea anapata
maumivu na hawezi kukupenda kwa kiwango
kinachotakiwa.
Hayo ni baadhi ya mambo ambayo unatakiwa
kuyazingatia kabla ya kurudiana na mpenzi wako
wa zamani. Cha kuzingatia sana ni kwamba
rudiana na mtu ambaye una imani
hamtakorofishana tena na kwamba kuachana
kwenu kwa mwanzo kuwe kumewapa fundisho.
Ni hayo tu marafiki, tukutane wiki ijayo kwa
mada nyingine.

No comments