JIHADHARI NA MZUNGU ‘ MPIGAPESA’ MJINI


TUNAENDELEA kuwapasha kuhusu baadhi ya
watu wanaotumia ujanja kuwaibia fedha
wananchi au wenyewe huita kupiga pesa .Njia
nyingi za watu kuibiwa fedha au mali zao
tumekuwa tukizieleza kwa kina katika safu hii
na wengi kuelimika na kukwepa mitego
inayofanywa na matapeli katika kuwaibia .

Leo tunaeleza mfano wa kweli ambao
umetokea mara kadhaa hapa jijini ambapo
watu wengi wamekuwa wakilizwa na tapeli
mmoja Mzungu . Jamaa yetu mmoja ambaye
naye ‘ alipigwa ’ fedha na Mzungu huyo
anasimulia hapa ilivyokuwa hata akajikuta
akitoa shilingi 200 , 000 kwa ‘ mtasha ’ huyo
kwa hiari yake na baadaye akagundua kuwa
ameibiwa kilaini . Ilikuwaje? Soma simulizi
yake.
“Nilikuwa Posta Mpya jijini Dar es Salaam
usiku ,” alianza kusimulia Bwana X ( nampa
jina la X kwa sababu aliomba jina lake
lisiandikwe gazetini ) .Baada ya kufika Posta
usiku aliamua kwenda kuchukua fedha ,
shilingi 200 ,000 kwenye ATM
moja. Alifanikiwa kwani baada ya kuingiza
kadi na kutoa fedha alipogeuka nyuma
akakutana na Mzungu mmoja na mambo
yakawa hivi :
“Dugu yangu nina shida kubwaa , ” alisema
yule mzungu .
“Una shida gani?”“ Gari yangu haina mafuta
nataka kubadilisha dola yangu. ”
“Sasa kama unataka kubadilisha dola mimi
nitakusaidiaje?”
“Nina dola mia mbili hapa , unajua thamani
yake ukibadili unapata shilingi laki tatu lakini
kwa kuwa nina shida nipe shilingi laki mbili ili
nitie mafuta , hiyo laki moja na kitu ni zawadi
yako , ” alisema Mzungu huyo kwa lafudhi ya
Kizungu .Bwana X alifikiria kwa sekunde
chache , akaona kwamba hawa ni wale
wazungu wenye roho nzuri . Shilingi laki
nzima anaacha ?
Haraka sana akaona ana bahati kubwa usiku
huo, hivyo alimtazama na akamuuliza”
“Hizo dola mia mbili ziko wapi ?”“ Zipo kwenye
gari yangu ile pale ,” alisema Mzungu
akionesha gari la rangi ya bluu lililokuwa
limeegeshwa hatua chache kutoka pale
alipokuwa .
Yule Mzungu alikwenda na kufungua mlango
akatoa begi kubwa . Alitoa burungutu la
fedha, dola za Kimarekani tupu na kuchomoa
noti za mia moja mbili na
kumkabidhi.“Umesema unataka shilingi laki
mbili tu , ” aliuliza Bwana X .“Nimesema hivyo ,
hiyo ziada ni shukurani yangu, ” akajibu.
“Haya basi hizi . ”
Mzungu baada ya kupokea fedha hakuwa na
haraka , alizihesabu na kuhakikisha kwamba
kweli zilikuwa shilingi laki mbili. Alimshukuru
yule bwana na akapanda kwenye gari lake na
kutoweka pale .
Jamaa aliondoka pale na kwenda Temeke
kwa rafiki yake akamsimulia rafiki yake jinsi
alivyompata Mzungu mwenye roho nzuri
usiku ule .
“Yaani dola mia mbili umempa shilingi laki
mbili tu ?”
“Kweli nakuambia , alikuwa na shida, gari lake
liliishiwa mafuta na hakukuwa na sehemu ya
kubadilishia , akasema hizo nyingine ni
zawadi yangu, ” alisema Bwana X.
Waliamua kwenda kubadili zile dola usiku
uleule ili wapate fedha za madafu na
walipofika kwenye duka la kubadilishia fedha
mambo yakawa hivi : “Haloo , hizo siyo dola, ni
makaratasi tu , ” alisema mwenye duka.
“Unasemaje ?” Aliuliza Bwana X huku akiwa
amepigwa na butwaa .
Akarudia alichokisema . Bwana X alikuna
kichwa na hakuamini kilichotokea .
Aliangaliana na rafiki yake bila kusema
neno.“Mbona mmepigwa na butwaa ?” aliuliza
mwenye duka.
“Tunashangaa kwa sababu aliyetupa fedha
hizo ni Mzungu , tena mwenye fedha zake na
gari la kisasa. ”
“Basi mrudieni mkamueleze , imekuwaje
amewapa dola feki ?” akashauri mwenye
duka.
Hawakuwa na la kufanya , baada ya kutoka
pale dukani walichokifanya ni kwenda Kituo
cha Polisi Oysterbay kwa kuwa kuna askari
mwenye cheo cha juu pale wanamfahamu , ili
kupata ushauri wa kipolisi.
Walipofika polisi na kuwafahamisha
kuhusiana na jinsi ‘ walivyopigwa’ fedha ,
polisi hawakuonesha kushangaa.
“Unajua hapa kuna taarifa nyingi tu
kuhusiana na Mzungu huyo , ameliza wengi, ”
alisema polisi yule .
“Sasa tumekuja hapa kupata ushauri , tufanye
nini?”“ Cha kufanya ni kuandika taarifa ili jeshi
la polisi limtafute kwa sababu anachofanya ni
uhalifu, tena makosa mawili . Kuwa na fedha
feki na kuibia watu hela zao,” alishauri polisi
yule.
“Kwani tangu hao wenzangu watoe taarifa ,
kwa nini hajakamatwa?”
“Ukweli ni kwamba hajanasa katika mtego
wetu, lakini anasakwa ,” akajibu.
Bwana X ilibidi aende kaunta na kuandikisha
maelezo yake kuhusiana na mzungu huyo.
“Acha namba yako ili akikamatwa tuweze
kukupigia ” alisema askari aliyekuwa
akiandika maelezo .
“Mkinipigia nikaja , tunampeleka
mahakamani?”“ Tutakupigia ili uje
kumtambua . Ukimuona si utamtambua ?”
“Hata iwe usiku wa manane , nitamtambua
kwa sababu wakati tunazungumza ile
sehemu ilikuwa na mwanga wa taa . ”Aliacha
na namba yake ya simu naye akaomba
namba ya yule askari aliyekuwa akiandika
maelezo yake . Hata hivyo ikawa ameibiwa .
Jihadharini sana na Mzungu huyu usije nawe
ukaibiwa !

No comments