CHADEMA YAENDELEA KUKOMAA YASISITIZA MAANDAMANO YAPO PALE PALE NCHI NZIMA
Mkurugenzi
wa Oganaizesheni, Mafunzo na Usimamizi wa Kanda wa Chama cha Demokrasia
na Maendeleo (Chadema), Benson Kigaila akisisitiza jambo kwa waandishi
wa habari.
Mkurugenzi
wa Oganaizesheni, Mafunzo na Usimamizi wa Kanda wa Chama cha Demokrasia
na Maendeleo (Chadema), Benson Kigaila akionesha barua za kuomba vibali
vya kufanya maandamano katika maeneo mbalimbali nchini.
Mkurugenzi
wa Oganaizesheni, Mafunzo na Usimamizi wa Kanda wa Chama cha Demokrasia
na Maendeleo (Chadema), Benson Kigaila (kushoto), akizungumza katika
mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam leo, kuhusu maandamano ya
chama hicho yatakayoanza kesho nchini kote kupinga Bunge Maalumu la
Katiba linaloendelea Dodoma. Kulia ni Kada wa Chadema, Aron Mashuve na
Mwanasheria wa chama hicho, John Malya.
Ofisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene akimkaribisha Kigaila kuzungumza na wanahabari.
Mwanasheria wa Chadema, John Malya akifafanua baadhi ya vipengere vya sheria kuhusu ruhusa ya kufanya maandamano.
Mwanasheria wa Chadema, John Malya akiwa na kada wa chama hicho, Aron Mashuve.
Wanahabari wakiwa kwenye mkutano huo.
CHAMA cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema), kimesisitiza kuwa migomo na maandamano yasiyokoma
nchi nzima yapo palepale na kwamba yanaanza rasmi kesho kwa kishindo
kikubwa na hakuna mtu wa kuyazuia kwani ni haki yao kikatiba.
Chadema kimesema lengo la maandamano hayo
ni kuishinikiza Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kitoe tamko la
kusitishwa Bunge Maalum la Katiba linaloendelea mjini Dodoma huku
likifuja fedha za wananchi.
Kauli hiyo ilitolewa jana Dar es Salaam
na Mkurugenzi wa Organizasheni na Mafunzo wa chama hicho, Benson
Kigaila wakati akizungumza na wanahabari Makao Makuu ya chama hicho
Kinondoni.
"Maandamano yaliyotangazwa na Freeman
Mbowe si ya kwake ni maazimio ya Mkutano Mkuu wa Chadema uliofanyika
Septemba 14, mwaka huu.
"Tunasisitiza kuwa maandamano na migomo
isiyokoma nchi nzima yapo palepale, lengo letu ni kuishinikiza Serikali
isitishe Bunge la Katiba kwani mkutano mkuu uliazimia jambo hilo baada
ya kuona kuwa kinachofanyika Dodoma hakitatupa Katiba Mpya, bali fedha
za wananchi zinatafunwa bure"alisema.
Aidha, alisema maandamano yao yapo
kisheria ambapo katika Katiba ya nchi, maandamano ni haki sheria namba 5
ya vyama vya siasa ya mwaka 1992 kifungu cha 11 kifungu kidogo cha 1
inaruhusu jambo hilo.
Kigaila aliongeza kuwa sheria hiyo
inataka waandamanaji kutoa taarifa ndani ya saa 48 kabla ya na si kuomba
kibali taratibu ambazo wao wameshazipitia.
"Natoa mwito kwa Watanzania wote wakatae
ufisadi unaofanywa na Bunge Maalumu la Katiba. Kilichoko Dodoma ni
kumaliza fedha ambazo zingetumika kujengea nyumba za walimu au hata
zahanati katika maeneo mbalimbali nchini,"alisema .
Kigaila alisisitiza kuwa wamepata barua
kutoka Jeshi la Polisi kuwataka kusitisha maandamano lakini
hawatasitisha kwa sababu, sababu za katazo hazina mashiko na hazijanukuu
kifungu chochote cha sheria.
Alisema licha ya wao Chadema, maandamano yao hayo yamepata baraka kutoka Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Mkurugenzi huyo wa organizasheni wa chama
hicho alisema maandamano hayo yanafanyika katika ngazi ya majimbo,
wilaya na mkoa, ambapo kwa mkoa yataanzia maeneo tofauti kuishia ofisi
za mkuu wa mkoa husika na kwa wilaya yatakwenda kwa mkuu wa wilaya
husika.
Alisema maandamano hayo kila mahali
yataanza asubuhi, huku kwa mikoa mitatu ya kanda ya Dar es Salaam
yataanza keshokutwa Jumatano.
Kwa upande wale Mwanasheria wa chama
hicho, John Mallya alisema sababu nyingine iliyotolewa na polisi kuwa
maandamano hayawezi kufanyika kwa sababu kesi iliyofunguliwa Saedy
Kubeinea ya kupinga Bunge hilo ipo mahakamani kuwa haina mashiko kwa
kuwa Chadema ni taasisi inayojitegemea na inamaamuzi yake ya kichama.
Post a Comment