Simba yamnasa straika mpya wa ukweli.. Soma habari kamili



SIMBA ipo katika hatua nzuri za kusajili kifaa kipya cha nane kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu Bara.
Mchezaji huyo ni straika Danny Lyanga ambaye amekuwa akihitajika na Yanga kila mara na kuidengulia kwa madai kwamba akili zake hazipo kwenye soka la Bongo.
Lyanga kwa sasa anaichezea FC Lupopo ya DR Congo ingawa hana mkataba nayo kwa madai kwamba mambo yao mengi yamekuwa magumashi na hawataki kumpa hela ya kueleweka, hivyo yuko katika mikakati ya kurudi kucheza soka nchini ndiyo maana Simba wakamwibukia fasta.
Endapo Simba watafanikiwa kupata saini ya Lyanga aliyewahi kung’ara na Coastal Union, basi atakuwa ni mchezaji wa nane katika usajili mpya unaowajumuisha Mussa Hassan ‘Mgosi’, Peter Mwalyanzi, Mohamed Fakhi, Samir Nuhu, Laudit Mavugo, Emery Nimubona pamoja na kipa wa JKU, Mohamed Abdulrahman ambaye bado hakijaeleweka kutokana na kubanwa wa mkataba wake uliobakiza mwaka mmoja na klabu yake.
Lyanga huenda akasaini Simba muda wowote kuanzia sasa baada ya vigogo hao kujiridhisha juu ya mkataba wake na Lupopo kama umemalizika na mchezaji huyo amewahakikishia kwamba yupo tayari kuja nchini ingawa amewambia kwamba akipata timu nje muda wowote wamruhusu aondoke jambo ambalo Simba wamekubaliana nalo.
Mchezaji huyo amewahi kuichezea Coastal Union misimu miwili iliyopita anatua Simba kuongeza changamoto kwa washambuliaji wenzake akiwemo Mgosi, Mavugo na Raphael Kiongera ambaye hana uhakika wa kurudi tena Simba.
Mmoja wa viongozi wa Simba, aliliambia Mwanaspoti akisema: “Mazungumzo yamefikia pazuri, kuna vitu tunamalizia kufuatilia ndipo tukamilishe kila kitu ila tunaamini atatusaidia endapo tutampata, lakini naamini muda wowote tutamalizana naye.”

No comments