
BAHATI yao. Hiyo ndiyo kauli ya Kocha wa Yanga,
Hans Van Der Pluijm na mwenzake Joseph Omog wa Azam FC baada ya timu zao kutoka sare ya mabao 2-2 jana Jumapili katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliofanyika Uwanja wa Taifa.
Matokeo hayo yanaifanya Mtibwa Sugar kuendelea kubaki kileleni mwa ligi hiyo ikiwa na pointi 16 baada ya jana asubuhi kutoka sare ya bao 1-1 na Stand United kwenye Uwanja wa Manungu, Turiani.
Yanga nayo imebaki nafasi ya pili na pointi zake 14 sawa na Azam iliyoko kwenye nafasi ya tatu. Yanga ipo juu kwa sababu ina wastani mzuri wa mabao, ikiwa imefunga mabao 11 huku ikiwa na mabao 10 tu.
Muda mfupi baada ya mchezo huo, Pluijm alisema: “Azam ni timu kubwa na timu yangu ilifanya makosa madogo madogo ambayo wenzetu wameyatumia na kusawazisha mabao yetu.
“Ni kama bahati yao kwani nimekaa na timu siku chache, lakini nimepata matokeo haya, kama ningekuwa na siku zaidi ningefanya vizuri.”
Kwa upande wake Kocha wa Azam, Omog alisema, siku zote mechi yake na Yanga huwa ngumu lakini anashukuru wachezaji wake wamejituma japo wapinzani wao walikuwa na bahati kwani kikosi chake kilipotea baada ya kupata bao la kwanza.
Azam ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya tano mfungaji akiwa ni Didier Kavumbagu aliyetumia vizuri makosa ya beki wa Yanga, Mbuyu Twite aliyeshindwa kuwasiliana vizuri na kipa wake, Deo Munishi ‘Dida’ katika harakati za kuokoa na kujikuta akimtulizia mpira mfungaji.
Straika mpya wa Yanga, Amissi Tambwe aliisawazishia timu yake dakika ya nane kwa kufunga bao la kichwa akimalizia krosi ya kiungo Salum Telela kutokea upande wa kulia wa uwanja. Timu hizo zilienda mapumziko zikiwa sare kwa bao 1-1.
Winga Simon Msuva aliifungia Yanga bao la pili kwa kichwa dakika ya 52 akiunganisha pasi ya kiungo Haruna Niyonzima, lakini straika wa Azam, John Bocco aliyeingia kuchukua nafasi ya Salum Aboubakari ‘Sure Boy’ aliisawazishia timu yake dakika ya 64 kwa kichwa akimalizia krosi ya Himid Mao.
Kama si papara ya kutaka kufunga, Kpah Sherman wa Yanga angeweza kuifungia timu yake dakika ya 22 baada ya kupokea pasi ya Tamwe na hata winga wa Azam, Brian Majwega alipiga krosi safi ambayo Kavumbagu alishindwa kuiunganisha dakika ya 15.
Katika mchezo huo, Azam iliwatumia wachezaji wake wapya, Majwega kutoka KCCA ya Uganda, Pascal Wawa (El Merreikh, Sudan) na Amri Kiemba aliyeingia kuchukua nafasi ya Kipre Tchetche. Yanga nayo iliwatumia wachezaji wake wapya, Tambwe, Sherman (Aries FC, Liberia) na Danny Mrwanda kutoka Polisi Moro.
Mchezo ujao Yanga itacheza na Mbeya City Jumamosi wiki hii huku Azam ikicheza na Mtibwa siku hiyo hiyo.
Post a Comment